Hospitali za umma Tanzania zatakiwa kupeperusha matangazo yanayohusu elimu ya afya

Mwanamke
Naibu Waziri wa Afya wa Tanzania Faustin Ndugulile amesema kuwa Watanzania wengi wana uelewa mdogo wa masuala ya Afya, jambo ambalo bado ni changamoto kubwa.
Akizungumza na BBC, bwana Ndugulile, amesema elimu ya kuhusiana na masuala ya afya bado ni ndogo kwa watanzania na kwamba wamekuwa wakibuni njia mbalimbali kuhakikisha elimu inatolewa kwa umma ili kuhakikisha kuwa watu wanayatambua magonjwa na kuweza kujikinga nayo.
Ametolea mfano, ongezeko la watu wenye magonjwa ya kisukari, shinikizo la damu na kwamba watu takriban laki moja na nusu wamebainika kuwa na ugonjwa wa kifua Kikuu, huku elfu 60, wakiwa tayari wamepatiwa tiba.
Dokta Ndugulile amesema kwa sasa kuna shida kubwa ya magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kiharusi, na kwamba magonjwa hayo kwa kiasi kikubwa yanahusiana na aina ya lishe, mazoezi na vileo watu wanavyokunywa.
Amesema katika hali kama hiyo kunahitajika kuendelea kutoa elimu ya afya, ikiwa sababu moja wapo pia ya kuwataka waganga wakuu wa mikoa yote nchini kuanza kutekeleza maelekezo ya Serikali.
Maelekezo hayo yanayoagiza runinga zote zilizofungwa kwenye hospitali za umma kurusha matangazo yanayohusu elimu ya afya.
'' Tumetaka kutumia ile fursa ambayo mtu ama mgonjwa anafika hospitalini wakati anasubiri kwenda kliniki basi awe anapata elimu, kuhusiana na maswala ya wajawazito, watoto na kisukari, shinikizo la damu. Makusudio ni kuhakikisha kwamba ule muda ambao mtu yuko hapo aweze kupata elimu ya masuala mbalimbali ya afya''. Amesema Dokta Ndugulile
Hata hivyo amefafanua kuwa agizo hilo ni kwa wagonjwa wa nje tu, ambaye anakuja kwa matibabu na kuondoka.
Ambaye anatumia muda mfupi ndani ya hospital.
''Kwa wagonjwa walio vitandani hili lina taratibu zake, kwa vile kuna wagonjwa wengine wanakaa zaidi ya miezi sita hospitali, sasa yule huwezi kuonesha ujumbe huo wa afya, utakuwa humtendei haki, wanahitaji nao kujua dunia inaendaje, tunazungumzi mgonjwa amnbaye anakuja kwa matibabu na kuondoka''
Aidha amesema licha ya tatizo walilokuwa nalo watu wazima wa afya iliyopitiliza lakini asilimia 34 ya watoto chini ya umri wa miaka mitano wana udumavu.
Naibu Waziri wa afya amesema elimu ya kutosha ikitolewa jinsi ya watu kujikinga nayo, taifa na watu wenyewe wataepuikana na gharama kubwa ya baadaye watakapoanza kujitibu magonjwa watakayoyapata ambayo wangeweza kuyazuia mapema.

Post a Comment

Previous Post Next Post