UPUNGUFU WA NGUVU ZA KIUME, SABABU NA TIBA.

 Image result for unhappy man
 Upungufu wa nguvu za kiume ni ugonjwa ambao mwanaume hushindwa kusimamisha uume na pia kushindwa kuendelea kubaki imara wakati wa tendo la ndoa.  Uume kusimama hutokea pale damu inapoingia katika tishu zilizo kama sponji na kuendelea kubaki ndani yake wakati wa tendo la ndoa.Hii hutokea kama matokeo ya mhemko kabla ya tendo la ndoa, ambapo taarifa hupelekwa kwenye ubongo na hatimaye taarifa hutumwa katika mishipa fahamu iliyo katika 
uume.
Sababu zinazosabisha tatizo hili zaweza kugawanywa kama ifuatavyo:-
 a)  Hitilafu katika ogani za mwili (Organic causes)
Hitilafu hizi ambazo zinatambulika zaidi ni kama magonjwa ya moyo na kisukari,upungufu wa homoni mwilini (kitaalam kama hypogonadism) ,maudhi yasiyotakiwa ya dawa mbalimbali(side effects), pia magonjwa ya mishipa ya fahamu yanayoweza kusababishwa na kuumia au kufanyiwa operesheni ya tezi dume.
Pia zifuatazo ni sababu nyingine katika kundi hili
  •  Kuziba kwa mishipa ya damu.
  • Kiwango kikubwa cha lehemu katika damu.
  • Unene (Obesity).
  • Kukosa usingizi.
  • Unywaji pombe kupindukia  na madawa ya kulevya.
  • Utumiaji wa tumbaku.
  • Kuumia kwa uti wa mgongo.  
  • Magonjwa ya mmeng’enyo.

b)Matatizo ya kisailolojia
Ubongo huwa na kazi maalum ya kuongoza jinsi viungo vya mwili vinavyofanya kazi, hii ni pamoja na kusimama kwa uume baada ya mhemko kabla ya tendo la ndoa. Kuna baadhi ya mambo yaweza kusababisha mwanaume asihemke na kuendelea kusababisha tatizo kuwa kubwa zaidi. Sababu hizo ni kama ifuatavyo:-


  •  Sononi, wasiwasi na hata magonjwa mengine yanayoathiri afya ya akili.
  • Msongo wa mawazo.
  •  Matatizo ya uhusiano ambayo hupelekea msongo wa mawazo, hata mawasiliano yaliyo duni.

c) Mchanganyiko wa hitilafu katika Ogani na Saikolojia kwa pamoja.

Tunavyoozeeka tatizo hili laweza kuongezeka, ingawa siyo hali ya kawaida mtu anapozeeka. Wazee ni kundi ambalo hutumia dawa za matatizo mbalimbali kwa wingi. Kwa hiyo tatizo hili la upungufu wa nguvu za kiume linapotokea mara nyingi huashiria hali ya kiafya isiyo ya kawaida au kusabishwa na aina fulani za dawa atumiazo mgonjwa. Mara nyingi hutokea kwa wale walio na miaka 60 na kuendelea. Hata hivyo vijana huweza pia kupata tatizo hili.

Pia wanaoweza kupata tatizo hili ni kama:-
  • Wenye matatizo ya kiafya, kama ugonjwa wa kisukari na ugonjwa wa moyo.
  •  Wenye kuendesha baiskeli kwa muda mrefu, uendeshaji wa baiskeli bila kutumia vifaa             maalum waweza kusababisha kukandamizwa kwa mishipa ya fahamu na kuathiri mzunguko      wa damu katika uume.
  •  Watumiaji wa dawa za kulevya pamoja na pombe, hususan watumiaji wa muda mrefu na                unywaji pombe kupindukia.
  •  Wenye msongo wa mawazo,sononi na wasiwasi
  •  Wenye kutumia aina mbalimbali za dawa.
  •  Waliojeruhiwa, hususan mishipa ya fahamu husika.
  • Wenye uzito mkubwa, hasa walio wanene.
  • Wenye kutumia tumbaku, ambayo huathiri mtiririko wa damu katika mishipa ya uume ya          ateri na veini.
Matatizo yenye kujitokeza ugonjwa usipotibiwa
  • Kutoridhika katika uhusiano.
  • Msongo wa mawazo na wasiwasi.
  • Sononi.
  • Kujisikia vibaya mbele ya jamii na kutokujiamini.
  • Matatizo ya uhusiano au kuvunjika kwa uhusiano.
  • Kutokuwa na uwezo wa kumpa ujauzito mwanamke.
Endapo tatizo hili litajitokeza, usikimbilie kuanza kutumia dawa, au kununua dawa katika famasi bila ushauri wa daktari. Dawa hazitakuwa na  msaada endapo chanzo cha tatizo hakijagundulika. Pia matumizi ya dawa yanaweza kukuletea athari nyingine kiafya, kama uchunguzi haukufanyika kwanza.

Jiandae kumwona daktari wako, kwa kukusanya taarifa mbalimbali kama dalili za ugonjwa ulizo nazo, listi ya dawa unazotumia, uwe na taarifa muhimu za kukuhusu, ni vyema ukienda na mwenzi wako kwa kuwa atakuwa msaada kwa yale uliyosahau na andaa maswali utakayomuuliza daktari wako.

Vipimo mbalimbali vyaweza kutumika ili kugundua sababu ya ugonjwa. Vipimo hivi hujumuisha vile vya kuchunguza mzunguko wa damu katika uume, pia kipimo maalum cha kuvaa nyakati za usiku kuchunguza mara ambazo uume unasimama ukiwa umelala, na vile vya kuchunguza viwango vya homoni mwilini.

Pia historia ya mgonjwa itamwezesha daktari kuweza kugundua tatizo la mgonjwa akishirikisha na vipimo mbalimbali tulivyovitaja hapo awali
  
Daktari ana wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa unapata tiba sahihi kulingana na kisababishi cha ugonjwa na kinachofanya hali kuwa mbaya kama tulivyoona awali.

Kulingana na sababu inayosabisha ugonjwa wa upungufu wa nguvu za kiume, unaweza kutibiwa kwa njia mbalimbali. Daktari wako na mfamasia watakuelezea faida na hasara ya kutumia tiba husika na watajali zaidi uamuzi wako. Pia mawazo ya mwenzi wako yatasaidia ili uweze kupata tiba iliyo sahihi.

Dawa za kumeza zinatumika sana katika kutibu upungufu wa nguvu za kiume na zimeonyesha mafanikio makubwa. Dawa hizi ni kama zifuatazo:-

a)  Dawa zinazoongeza mzunguko wa damu katika uume,

  •          Tadalafil(Sialis)
  •          Sildenafil (Viagra)
  •          Verdenafil ( Levitra)
  •          Avanafil (Stendra)
Tahadhari
Chukua tahadhari kabla ya kutumia dawa yeyote kutibu nguvu za kiume, hata kama ni dawa za kienyeji au zile zinazonunuliwa bila ya kuandikwa na daktari. Wasiliana na mfamasia kwa ushauri zaidi.

Dawa zitumiwapo ovyo zinaweza zisikusaidie kutatua tatizo na zaweza kuwa hatari kama:-
  • Unatumia dawa zenye nitrate-ambazo huandikiwa wagonjwa wenye maumivu ya kifua (angina), kwa mfano Nitroglycerin,Isosorbide mononitrate na isosorbide dinitrate.
  • Unameza dawa za kusaidia mtiririko wa damu (anticoagulant) au dawa za shinikizo la juu la damu.
  •  Una tatizo la moyo au moyo kushindwa kufanya kazi.
  •   Una ugonjwa wa kiharusi au uliwahi kupata kiharusi.


b)      Dawa za homoni.
Dawa kama testosterone yaweza kutumika kwa wanaume wenye upungufu wa homoni hiyo. Kwa wale wenye upungufu wa homoni dawa hii inaweza kuwa tiba ya kwanza

Upasuaji waweza kufanyika endapo mishipa ya damu ya uume itakuwa imeziba na kusababisha upungufu wa nguvu za kiume.

Ushauri nasaha ni muhimu kwa wagonjwa wenye matatizo ya kisaikolojia, ambayo hupelekea msongo wa mawazo, wasiwasi na hata sononi. Daktari wako anaweza kukushauri wewe na mwenzi wako kuonana na mwanasaikolojia au mshauri nasaha kama tatizo hilo linaleta mvurugano katika uhusiano wenu

Post a Comment

Previous Post Next Post